Tanzania inategemea kuwa mwenyeji wa mkutano wa Kazi kujadili mpango wa uwekezaji katika sekta ya kilimo kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 10 hadi 11 Novemba mwaka huu, hayo ni kwa mujibu wa Msimamizi wa Misaada ya Maendeleo na Uratibu wa Mashirikiano wa Kimataifa katika sekta ya kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Margaret Ndaba .
Ndaba amesema zaidi ya wajumbe 200 wanategemea kuhudhuria mkutano huo kutoka ndani na nje ya nchi ambao ni wadau wakubwa wa sekta ya kilimo.
Alizitaja tasisi zitakazoleta wajumbe wake kuwa ni wizara za sekta ya kilimo hapa nchini, wizara zinazofanyakazi na wizara za sekta za kilimo kama Wizara ya Miundo Mbinu, Fedha, Ardhi na Mandeleo ya Makazi, Makamu wa Rais na Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto.
Wizara nyingine alizitaja kuwa ni wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mawasiliano na Uchukuzi, Elimu na Ufundi na wizara ya Sayansi na Teknolojia.
Pia wajumbe wa mkutano watatoka Sekta binafsi, Asasi zisizo za kiserikali, Muungano wa vyama vya Ushirika, Wabia wote waliosaini makubaliano ya kuendeleza sekta ya kilimo hapa Tanzania ( Tanzania CAADP Compact).
Wadau wakubwa wa kilimo ambao pia ni walengwa wa mkutano huu Wakulima, wataalikwa kupitia Muungano wa vikundi vya Wakulima (MVIWATA).
Tasisi zitakazo kuwa na wajumbe wake kutoka nje ya nchi kuwa ni pamoja na Umoja wa Africa ( AU), Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP).
Tasisi nyingine za nje zitakazoleta wajumbe wake katika mkutano huo kuwa ni pamoja na NEPAD, wawakilishi wa kanda za SADC, Jumuia ya Afrika mashariki na jumuia ya COMESA.
Washirika wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi pia wamealikwa katika mkutani huo, ambao aliwataja kuwa ni Shirika la Misaada Marekani (USAID), Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Wawakilishi wa balozi za nje hapa nchini.
Alisema lengo kubwa la mkutano huo ni kujadili mpango mzima wa kuendeleza sekta za kilimo hapa nchini ili kuleta mapinduzi ya kweli katika kilimo kwa siku za usoni na hasa wakati huu wa utekelezaji wa azma ya Kilimo Kwanza.
Mada zitajikita zaidi kujadili mpango wa kuendeleza kilimo , utekelezaji wake na gharama husika ambapo serikali na wadau wake mbali mbali watahitajika kutoa matamko ya uchangiaji wa mpango huo, aliongeza Ndaba katika mazungumzo yake.
“Mkutano huo wa siku mbili utafanyika katika hoteli ya Hyatt Regency, Jijini Dar Es Salaam na wenyeviti wake watakuwa Mkamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dr Gharibu Bilali katika siku ya kwanza ya mkutano na siku ya pili ya kikao kitaendeshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Jakaya Kikwete “ , alimalizia Ndaba.