Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe amekutana na wazalishaji na wasambazaji wa sukari na kuwaagiza kuacha mara moja kusafirisha sukari kwa njia ya magendo na kuiuza nchi za jirani kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi.
Waziri Maghembe alisema si vyema hata kidogo kwa wazalishaji kuzalisha sukari na kisha kuiuza kwa magendo nje ya nchi kwani huo si utaratibu na ni kukiuka sheria na masharti ya leseni walizopewa.
Waziri Maghembe aliwaambia wazalishaji hao kuwa uzoefu aliokuwa nao ni kuwa sukari imepanda kwa kiwango cha juu. Alitoa mfano wa Mkoani Kilimanjaro wiki mbili zilizopita hali ilikuwa mbaya zaidi kwani sukari ilikuwa haipatikani kabisa na kuongeza kuwa matatizo ya kusari kuadimika na inapopatika inauzwa kwa bei ya juu kwa sababu ya wazalishaji na wasambazaji kutokuwa waaminifu kwa Serikali iliyowapa leseni na kuwajengea mazingira mazuri ya wao kuiongoza Sekta ndodo ya Sukari.
Waziri Maghembe alisema wiki hii alifanya ziara katika masoko kadhaa, Jijini Dar es Salaam katika Wilaya ya Temeke, ambapo katika maduka mengi sukari ilikuwa ikiuzwa kwa Shilingi 2,600 kwa Kilo moja na mfuko mmoja wa Kilogramu 50 ulikuwa ukiuzwa kati ya Shilingi 85,000 na Shilingi 105,000.
Waziri Maghembe aliwaambia wazalishaji hao kuwa hali imekuwa hivi kwa sababu Serikali iliamua kwa dhati kulinda soko la ndani na ilifanya hivyo kwa nia nzuri kwa kuwa katika nchi kama Tanzania ambayo sekta binafsi inaendelea kukua ni vyema kulinda viwanda vya ndani na kuonya kuwa kama Wazalishaji hao wakiendelea na hali hii basi Serikali itafikiria utaratibu mwingine.
“Haiwezekani Watanzania wanunue sukari kwa foleni, hii haikubaliki na kamwe Serikali haiwezi kuangalia mambo yakiwa yanaharibika kwa kiwango hiki, ni lazima wazalishaji na wasambazaji muhakikishe Watanzania hawaingii kwenye matatizo” Alikaririwa Waziri Maghembe.
Wazairi Maghembe aliwaambia wazalishaji na wasambazaji hao kuwa Serikali ipo kutekeleza wajibu wake ambao ni kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na mambo mengine kama kutoa vibari vya kuuza sukari kwa utaratibu maalum na si magendo kama ilivyo sasa.
“Tuna ushahidi kuwa sukari iliyo kwenye akiba ya wafanyabiashara ni kidogo kwa kuwa imekuwa ikisafirishwa kwenda nchi jirani kimagendo. Alitoa mfano wa takwimu alizopewa wiki mbili zilizopita zilionyesha kuwa Kilombero Sugar na mfanyabiashara Mohamed Enterprises walikuwa na akiba ya tani 2,300 tu tofauti na uzalishaji ambao huwa ni akiba ya tani 30,000 kwa mwezi na kuongeza kuwa upo ushahidi unaoonyesha kuwa kiwango kikubwa cha sukari inauzwa nje ya nchi.
Akiongea kwa niaba ya Wazalishaji wa Sukari Bwana Ahmad Yahya kutoka Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa alisema sukari imekuwa ikipanda kwa sababu mahitaji ya sukari yamekuwa makubwa na pili wazalishai wamekuwa wakitumia gharama kubwa za uzalishaji. Alizitaja gharama hizo kuwa kupanda kwa bei ya mbolea kutoka Dola 300 mpaka dola 700, bei ya chuma nayo imepanda mara mbili zaidi sambamba na gharama za nishati ya umeme kwa kuwa kumekuwa na tatizo la mgao wa umeme ambalo limechangia gharama ya nishati kupanda mara tatu zaidi ukilinganisha kama wangekuwa wakitumia umeme wa gridi ya taifa.
Waziri Maghembe aliafiki maelezo hayo lakini aliwakumbusha kuwa sababu hizo zilishajadiliwa katika Mkutano alioitisha Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Peter Pinda ambapo baada ya mkutano huo kwa kauli moja wazalishaji walikubali bei ya sukari iuzwe kwa Shilingi 72,000 kwa mfuko wa Kilo 50 bei hiyo ni bila VAT ili na wafanyabisha wanaouza rejareja wakinunua kwa bei hiyo wauze si zaidi ya Shilingi 1,700 kwa Kilo Moja, bei ambayo Watanzania wengi wanaimudu.
Baada ya kusikiliza hoja zao Waziri Maghembe alitoa tamko la Serikali kwa wazalishaji na wasambazaji hao kama ifuatavyo: - Moja Serikali imeruhusu Sukari kiasi cha Tani 100,000 iingizwe mara moja na utaratibu wa vibali utasimamiwa na kuratibiwa na Bodi ya Sukari.
Pili, Lazima Wazalishaji na wasambazaji wauze sukari yao ndani ya nchi ili kumpa unafuu Mtanzania na kama wanataka kuuza sukari nje ya nchi basi waombe vibali vya kufanya hivyo lakini atakayekiuka Serikali itachukua hatua ya kuyakamata magari yanayosafirisha sukari kwenda nchi jirani na kuitaifisha suakari pamoja na magari yalihusika kwenye biashara hiyo ya magendo.
Tatu, Bodi ya Sukari iandae mkutano wa kuwakutanisha Wadau wa sukari kabla ya tarehe 20 Oktoba, 2011.
Nne, Wasambazaji watakaopewa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi mara watakaponunua sukari hiyo watatakiwa kuonyesha shehema ya sukari waliyoagiza chini ya ukaguzi wa Bodi ya Sukari.
Tano, Serikali inawasiliana na Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania ili kuongeza idadi ya wasambazaji kwa kila Mkoa lakini kwa kuwachagua walio waaminifu tu.
Na mwisho, wazalishaji na wasambazaji kuwa waaminifu kwa kuuza sukari kwa bei elekezi iliyotolewa na serikali yaani Shilingi 72,000 bila VAT kwa mfuko wa Kilogramu 50. Utekelezaji wa maazio hayo unaanza mara moja alisisitiza Waziri Maghembe.
No comments:
Post a Comment